top of page
Art%C3%ADculosA-Dar%C3%ADo1_edited.jpg

UTAMBULISHO WA DARIO, MMEDI

Profile-StevenAnderson.jpg

Steven D. Anderson, Ph.D.  | Oktoba 7, 2020

Imetafsiriwa na: Patrick Salvatory na Esther Mwanisi | Desemba, 2020

Kitabu cha Biblia cha Danieli kinamuelezea mfalme aliyeitwa “Dario, Mmedi,” mtoto wa Ahasuero, ambaye aliyechukua utawala dola mpya ya Babeli baada ya Babeli kushindwa na jeshi la umedi na Uajemi (Danieli 5:31). Dario, Mmedi, ndiye mhusika mkuu katika Danieli 6, na maono ya Danieli 9 yanasemekana kutokea wakati wa utawala wake. Hata hivyo, shida inatokea wakati wa kujaribu kumtambua Dario, Mmedi, katika vitabu vya zamani visivyo vya kibiblia. Kulingana na vyanzo visivyo vya kibiblia, mtazamo wa makumbaliano wa wanahistoria wa kisasa ni kwamba Koreshi, Mwajemi, aliishinda Umedi mwaka wa 553 KK na kumwondoa madarakani mfalme wa mwisho wa Umedi. Kulingana na tafsiri hii ya kihistoria, Koreshi, kama mfalme wa Uajemi, alitawala kama mtawala mkuu wa dola yote ya Umedi na Uajemi wakati Babeli ilipoanguka mnamo 539 KK.


Wasomi wameijibu shida ya kumtambua Dario, Mmedi, katika vyanzo visivyo vya kibiblia katika njia saba zilizoelezwa hapo chini.

Dario, Mmedi, kama uzushi
Maelezo ya mtazamo: Mtazamo huu unakanusha uwepo wa kihistoria wa Dario, Mmedi, na historia ya kitabu cha Danieli.


Watetezi: Huu umekuwa mtanzamo uliokumbaliwa kati ya wasomi wakosoaji tangu sehemu ya mwisho ya karne ya kumi na tisa, ingawa kuna wasomi wachache wanaokosoa ambao wanafuata moja kati ya mtazamo wa kihistoria wa kumuona Dario, Mmedi, kama mtu wa kihistoria. Mifano ya watetezi wa Dario, Mmedi, kama uzushi ni pamoja na Driver, Rowley na Grabbe.


Sababu: Mtazamo huu una hoja za aina mbili, za kihistoria na kithiolojia. Hoja ya kihistoria ni kuwa kuna vyanzo visivyo vya kibiblia ambavyo vinaeleza tafsiri ya kihistoria ya Koreshi ambayo haitambui uwepo wa Dario, Mmedi. Chanzo kikuu nje ya Biblia ambacho wakosoaji wake wanaunga mkono suala la Dario, Mmedi, ni mwanahistoria Mgiriki Herodoti (Herodoto). Maandishi ya kikabari mbalimbali vya zamani yamenukuliwa kama uthibitisho wa Herodoti. Wakosoaji wengi wanadai tu kwamba vyanzo hivi vinathibitisha kutokuwepo kwa Dario, Mmedi, bila kushughulikia utambulisho wa Dario, Mmedi, uliopendekezwa na wasomi wengine. Kimsingi wakosoaji hao wanakataa kitabu cha Danieli kama chanzo cha kihistoria. Hii ni kutokana na sababu za kithiolojia: Wakosoaji hao wanatamani kuthibitisha kwamba kitabu cha Danieli sio neno la Mungu, lakini kimsingi ni kazi ya kubuni. Hivyo kila wakati vyanzo visivyo vya kibiblia vinaonekana kupingana na maelezo katika kitabu cha Danieli, wakosoaji hawa wameweka uaminifu yao katika vyanzo hivi vya ziada vya kibiblia na kukanusha kile kitabu cha Danieli kinavyosema.


Pingamizi #1: Mtazamo huu una hoja za kithiolojia, na kwa sababu hii haukichukulii pasipo upendeleo kitabu cha Danieli lakini badala yake unataka kukipinga. Nia na utangulizi wa wakosoaji unaamua hitimisho lao.


Pingamizi #2: Mtazamo huu na vyanzo vingine vya kale ambavyo havimuelezei Herodoti kwa maelezo ya kina zaidi, hii inasababisha kutambua ubaguzi na utata katika vyanzo hivi.


Pingamizi #3: Mtazamo huu lazima ukanushe sio tu historia ya kitabu cha Danieli, bali pia vyanzo mbalimbali vya ziada vya kibiblia ambavyo vinaonekana kukubaliana na kitabu cha Danieli. 


Pingamizi #4: Mtazamo huu hautambui uwezekano wa mahusiano ya kiutawala kati ya Koreshi na Dario, Mmedi, ambao ungeruhusu utawala wa Dario, Mmedi, kipindi cha utawala wa Koreshi.


Pingamizi #5: Mtazamo huu hauwezi kukubaliwa na mtu ambaye anaamini Biblia, kwani unapinga waziwazi uthibitisho uliofanywa katika kitabu cha Danieli. 

Dario, Mmedi, kama Gubaru 
Maelezo ya mtazamo: Mtazamo huu unamfananisha Dario, Mmedi, na Gubaru au Ugbaru gavana wa Gutium ambaye aliungana na Koreshi na aliitwa gavana wa Babeli na Koreshi.


Watetezi: Wasomi wengi wa kiinjili walioandika katika robo tatu za kwanza za karne ya ishirini waliunga mkono nadharia hii. Maelezo ya kawaida ya mtazamo huu yalitolewa na Whitcomb. Shea aliuboresha mtazamo huu kwa kujibu matatizo yaliyopatikana katika uundaji wake. 


Sababu: Nadharia hii iliundwa baada ya ugunduzi wa maandishi mbalimbali ya kikabari ambayo yalizingatia uthibitisho wa hadithi ya Koreshi katika toleo la Herodoti. Katika kutafuta kwao takwimu za toleo hili la hadithi kwamba nani angeweza kufanana na Dario, Mmedi, wasomi wengi wa kiinjili walimfananisha Dario na Gubaru (pia aliitwa Ugbaru na Gobryas). Mtu huyu alitajwa na Xenophon (Zenofono), historia ya Nabonido (Nabonidi) na maandiko ya mikataba ya Babeli. Aliteuliwa kuwa gavana wa Babeli na Koreshi, na kwa sababu ya nafasi yake ya juu Gubaru alifananishwa na Dario, Mmedi. Nadharia hii kwa sehemu imejikita katika utambulisho wa “milki ya Wakaldayo” (Danieli 9:1) pamoja na nchi ya Wakaldayo, ingawa kwa uhalisia milki wa Wakaldayo ulizunguka eneo kubwa zaidi kuliko Babeli.


Nadharia ya Whitcomb na udhaifu wake: Whitcomb alisema kuwa Gubaru alikuwa ni mtu tofauti na Ugbaru kwa sababu historia ya Nabonido inasema kuwa Ugbaru alikufa wiki tatu baada ya anguko la Babeli. Na kwa Gubaru, maandiko ya mikataba ya Babeli ya mwaka wa nne wa Koreshi hadi mwaka wa tano wa Kambesi yanamtaja Gubaru kama gavana wa Babeli. Whitcomb alimfananisha Dario, Mmedi, na gavana huyu aliyeitwa “Gubaru.” Shida ni kwamba Whitcomb alidhania kuwa Gubaru pia alikuwa gavana wakati wa miaka ya mwanzo ya utawala wa Koreshi. Hata hivyo maandishi ya mkataba yanamtaja mtu tofauti kama gavana wa Babeli wakati wa miaka hiyo na mtu huyo alikuwa gavana huyohuyo wa Babeli ambaye alikuwa gavana kabla ya kuanguka kwa Babeli. Hivyo, Gubaru wa Whitcomb hawezi kuwa mtu aliyepokea ufalme mara tu baada ya anguko la Babeli (Danieli 5:31).


Nadharia ya Shea na udhaifu wake: Shea alisema kuwa mtu aliyeitwa “Ugbaru” katika historia ya Nabonido ni yule yule ambaye historia inamuita “Gubaru” na Shea anamfananisha Dario, Mmedi, na mtu huyo. Hata hivyo taarifa kutoka kwenye historia inaongeza kwenye hitimisho kuwa Gubaru hakuweza kushikilia nafasi ya utawala kwa zaidi ya wiki moja baada ya kuanguka kwa Babeli. Hii ni kwa sababu Koreshi aliingia Babeli wiki mbili baada ya anguko la mji, na Shea alidhani kwamba Koreshi alimwita Gubaru gavana kwa kipindi hiko. Hata hivyo, Gubaru alikufa siku nane baadaye. Shea anajaribu kusema kuwa matukio yote ya Danieli 6 na 9 yangeweza kutokea kwa wiki moja tu lakini hii ni hoja ngumu sana kuelezewa.


Pingamizi la jumla #1: Hakuna ushahidi kuwa “Gubaru” aliitwa Dario.


Pingamizi la jumla #2: Hakuna ushahidi kuwa baba wa Gubaru aliitwa “Ahasuero” (jina la kifalme).


Pingamizi la jumla #3: Mtu aliyeitwa “Gobryas” na Xenophon anafanana kabisa na mtu anayeitwa “Gubaru” na “Ugbaru” katika Kitabu cha Nabonido, na Xenophon anasema kwamba mtu huyu alikuwa “Muashuru,” ambaye ni, mzaliwa wa Babeli. Haiwezekani kudhibitisha kuwa Gubaru alikuwa Mmedi bila kupingana na Xenophon.


Pingamizi la jumla #4: Hakuna chanzo cha ziada cha kibiblia kinachoelezea Gubaru kama “mfalme.” Ingawa Danieli 6:1-7 hutumia maneno ya Kiaramu mawili kwa neno “gavana” (פחה na אחשדרפן) kwa mara kadhaa, maneno haya hayatumiki kamwe kwa Dario, Mmedi. Badala yake, kitabu cha Danieli kinatumia neno “mfalme” kwa Dario, Mmedi, mara thelathini, na katika Danieli 6:25-27 Dario anatoa amri kwa ulimwengu mzima. Ni ngumu kuona ni kwa jinsi gani Dario, Mmedi, angeweza kuwa gavana wa kawaida tu.


Pingamizi la jumla #5: Katika Danieli 6:7-9, Dario, Mmedi, anatoa amri ambayo inakataza mtu yeyote kutoa ombi kwa Mungu au mtu yeyote isipokuwa yeye mwenyewe. Amri kama hiyo ingeweza kutolewa tu na mteule mwakilishi wa hadhi ya juu kabisa katika ufalme, na sio na gavana. Hii inathibitishwa na Danieli 6:8, 12, 15, ambayo inasema kwamba hakuna mtu katika ufalme angeweza kubatilisha amri iliyotolewa na Dario, Mmedi. Hivyo, kitabu cha Danieli chenyewe kinapingana na nadharia zote zinazomtambulisha Dario, Mmedi, kama gavana wa kawaida.

Dario, Mmedi, kama Koreshi
Maelezo ya mtazamo: Mtazamo huu unamtambulisha Dario, Mmedi, na Koreshi, mfalme wa Uajemi.


Watetezi: Nadharia hii ilikuwa maarufu kwa wasomi wa kiinjili walioandika katika sehemu ya mwisho ya karne ya ishirini, kuanza na Wiseman mnamo 1965.


Sababu: Mtazamo huu unaweza kukubali toleo la kawaida la hadithi ya Koreshi na bado unathibitisha uhalisia wa kihistoria wa Dario, Mmedi. Ina faida ya kumtambulisha Dario na mtu ambaye bila shaka alikuwa na cheo cha “mfalme” baada ya anguko Babeli. Kulingana na nadharia hii, Danieli 6:28 inapaswa kutafsiriwa, “Basi Danieli huyu akafanikiwa katika enzi ya Dario, hii ni, katika enzi ya Koreshi, Mwajemi” (taz. 1Ny. 5:26). Mama wa Koreshi alikuwa binti wa mfalme wa Umedi Astyages, na kwa hivyo Koreshi angeweza kuitwa “Mmedi” au “Mwajemi.”


Pingamizi #1: Kitabu cha Danieli kila wakati kinatofautisha kati ya “Koreshi, Mwajemi,” na “Dario, Mmedi.” Hakuna ufafanuzi mzuri wa matumizi ya majina haya mawili na maelezo katika kitabu cha Danieli ikiwa yote yanamaanisha mtu yule yule.


Pingamizi #2: Katika maandishi yake, Koreshi kila wakati anajitambulisha kama Mwajemi, sio Mmedi.


Pingamizi #3: Hakuna uthibitisho wa nje ya Biblia kwamba Koreshi aliitwa “Dario” au kwamba baba yake (Kambisi I) aliitwa “Ahasuero.”


Pingamizi #4: Herodoti, Xenophon, na silinda ya Nabonido wanatoa taarifa ambazo zinaonyesha kwamba Koreshi alikuwa chini ya umri wa miaka 62 wakati aliposhinda na kuichukua Babeli, ambayo haiendani na maelezo ya Dario, Mmedi, katika Danieli 5:31.


Pingamizi #5: Mtazamo huu unakubali historia ya kawaida ya Koreshi bila shaka-kwamba, inafuata tu historia ya Herodoti na vyanzo ambavyo vinaonekana kukubaliana na Herodoti. Haizingatii uwezekano wa kuwa vyanzo vingine vya nje vya Biblia ambavyo vinasema hadithi tofauti vinaweza kuwa sahihi.

Dario, Mmedi, kama mtu wa kihistoria, lakini asiye na utambulisho wa uhakika
Maelezo ya mtazamo: Mtazamo huu unathibitisha kwamba Dario, Mmedi, alikuwa ni mtu halisi kihistoria, lakini haiwezekani kujua alikuwa nani katika vyanzo vya nje ya Biblia.


Watetezi: Haya yalikuwa maoni ya E. B. Pusey katika sehemu ya mwisho ya karne ya kumi na tisa. Katika sehemu ya mwisho ya karne ya ishirini, wafasiri wengi wa kiinjili walipitisha maoni haya.


Sababu: Mtazamo huu unatambua matatizo ya ufananisho wa Dario, Mmedi, na Gubaru / Ugbaru, na vile vile ufananisho wa Dario, Mmedi, na Koreshi, lakini hata hivyo unakazia msukumo na mamlaka ya kitabu cha Danieli. Watoa maoni ambao hawakujua ni nadharia gani inayoweza kuwa ndiyo sahihi, lakini ambao hata hivyo walikuwa na hakika juu ya uaminifu wa kitabu cha Danieli, wakakubali maoni haya.


Pingamizi: Maoni haya yanaweza kuwa halali katika hali zingine, lakini kwa zingine inaweza kuonyesha mtazamo wa kutojali kuhusu madai ya sehemu ngumu kihistoria katika Biblia.

Dario, Mmedi, kama Kambisi II
Maelezo ya mtazamo: Mtazamo huu unamfananisha Dario, Mmedi, na Kambisi II, mwana na mrithi wa Koreshi.


Mtetezi: Kuna msomi mmoja tu ambaye amependekeza nadharia hii, Charles Boutflower.


Sababu: Kuna maandishi ya kikabari ambayo yanamuelezea Kambisi II kama aliyetawal pamoja na Koreshi katika kipindi cha mwaka wa kwanza baada ya anguko la Babeli. Kwa kuwa Kambisi alipewa jina la “mfalme,” angeweza kutimiza jukumu la Mfalme Dario ambaye alipokea ufalme mpya wa Babeli baada ya anguko la Babeli (Danieli 5:31).


Pingamizi #1: Majina hayalingani. Hii ni kwasababu, hakuna ushahidi kwamba Kambisi aliitwa “Dario,” au kwamba baba yake Koreshi aliitwa “Ahasuero.”


Pingamizi #2: Ingawa mama yake Koreshi alikuwa Mmedi, Kambisi na baba yake siku zote wanaitwa Waajemi, sio Wamedi, katika vyanzo vya nje vya Biblia.


Pingamizi #3: Kambisi asingeweza kutoa amri za Danieli 6:7-9 na 6:25-27 wakati baba yake alikuwa mtawala mkuu.


Pingamizi #4: Kambisi alikuwa chini ya umri wa miaka 62 wakati wa anguko la Babeli, ambayo hailingani na maelezo ya Dario, Mmedi, katika Danieli 5:31. Boutflower anapendekeza kwamba maandishi ya asili ya Kiaramu ya aya hii yalibadilishwa, lakini hakuna ushahidi wowote wa maandishi kuunga mkono maoni haya.
 


Dario, Mmedi, kama Astyages
Maelezo ya mtazamo: Mtazamo huu unamfananisha Dario, Mmedi, na Astyages, babu wa mama yake Koreshi.


Watetezi: Ni wasomi wachache tu waliopendekeza nadharia hii, pamoja na John Lightfoot, Westcott, na Alfrink. Inaonyeshwa pia katika aya ya kwanza ya kitabu cha apocrypha cha Bel na Dragon.


Sababu: Herodoti anasema kuwa Astyages alikuwa mfalme wa mwisho wa Wamedi na hakuwa na mtoto wa kiume. Ikiwa mtu atakubali dai hili, basi ni sawa kujaribu kumtambua Dario, Mmedi, kama Astyages. Herodoti anasema kwamba Koreshi alimwondoa Astyages, lakini hakumuua. Inaweza kudhaniwa kuwa Astyages alirejeshwa kwenye ufalme na Koreshi wakati Koreshi alimfanya mwanawe Kambisi kuwa mtawala pamoje naye. Katika hali hii, Astyages angefanywa mtawala pamoje naye wa tatu ili kuwa mwalimu wa Kambisi, na angeweza kupewa jina la kiti cha enzi “Dario.”


Pingamizi #1: Mtazamo huu unapingana na Xenophon, ambaye anathibitisha kuwa Astyages alikufa kabla ya Koreshi kuanza kampeni zake za mapambano. Xenophon anathibitisha zaidi kuwa Astyages alirithiwa na mtoto wake wa kiume aliyeitwa Kuazari (Cyaxares), ambaye alitawala kama kiongozi na Koreshi. Vyanzo vinavyomuunga mkono Xenophon pia ni ushahidi dhidi ya ufananisho wa Dario, Mmedi, na Astyages.


Pingamizi #2: Mawazo yaliyotolewa na mtazamo huu ni ya kukisia tu, ikizingatiwa kuwa hakuna chanzo chochote cha kale kinachosema chochote juu ya kurudishwa kwa Astyages kwenye kiti chake cha enzi.

Dario, Mmedi, kama Kuazari (Cyaxares) II
Maelezo ya mtazamo: Mtazamo huu yanamfananisha Dario, Mmedi, na Kuazari II, mwana na mrithi wa Astyages kulingana na mwanahistoria wa Ugiriki Xenophon.


Watetezi: Huu ulikuwa mtazamo wa wasomi wengi wa Kiyahudi na Kikristo kutoka kwa Josephus na Jerome hadi Keil mnamo miaka ya 1870, lakini uliachwa baada ya kugundulika kwa maandishi ya kikabari ambayo yalionekana kuunga mkono hadithi ya Herodoti ya kutawazwa kwa Koreshi, ambayo hairuhusu uwepo wa Kuazari II ulioelezewa na Xenophon. Walakini, maelezo ya Kuazari II katika Cyropaedia ya Xenophon yanalingana vizuri na maelezo ya Dario, Mmedi, katika kitabu cha Daniel. Kwa kuwa utambulisho wa Dario, Mmedi, ambao unategemea toleo la kihistoria la Herodoti una udhaifu mwingi, ufananisho wa Dario, Mmedi, na Kuazari II umerudi kwa wasomi wa Biblia. Mimi (Steven Anderson) niliandika tasnifu yangu ya udaktari (2014; pdf, pdf, kitabu cha kuchapisha) juu ya mada ya Dario, Mmedi, nikitetea kufananishwa kwa Dario, Mmedi, na Kuazari II. Wasomi wengine wa kiinjili, kama Kirk MacGregor na Paul Tanner, baadaye walifuata hoja zangu.


Sababu: Xenophon anamuelezea Kuazari II kama mfalme wa mwisho wa Wamedi na mjomba wa Koreshi. Kulingana na Xenophon, Kuazari II alikuwa mfalme wa Umedi na Koreshi alikuwa mfalme wa Uajemi, na wote wawili walikuwa washirika katika serikali moja iliyoshirikishwa. Mpangilio huu wa kugawana mamlaka unatoa njia ya kupatanisha maandiko ya kibiblia (kwa mfano, Isaya 45:1-3) na maandiko mengine ya kibiblia ambayo yanamuelezea Koreshi kama kiongozi mkuu wa ufalme na uthibitisho wa kitabu cha Danieli kwamba kulikuwa na mfalme aliye juu kuliko Koreshi wakati wa anguko la Babeli. Kulingana na Xenophon, Kuazari II aliishi kwa miaka miwili baada ya anguko la Babeli, ambao ni muda wa kutosha kwa matukio ya Danieli 6. Kwa kuwa Kuazari hakuwa na mrithi wa kiume na Koreshi alikuwa amemwoa binti yake, Koreshi alirithi nafasi ya Kuazari baada ya kifo chake na kuungana falme za Umedi na Uajemi kama ufalme mmoja. Ingawa Xenophon anatumia tu jina “Kuazari,” kuna ushahidi kutoka vyanzo vingine kwamba Kuazari alitwaa jina la ufalme “Dario.” Pia kuna ushahidi kwamba baba wa Kuazari, aliyeitwa “Astyages” na mwanahistoria wa Ugiriki, alichukua jina la kifalme “Ahasuero” (= Xerxes). Xenophon hatoi umri halisi wa Kuazari, lakini uthibitisho wake kwamba Kuazari alikuwa mzee kuliko Koreshi unafanana na uthibitisho katika Danieli 5:31 kwamba Dario, Mmedi, alikuwa na umri wa miaka 62 wakati wa anguko la Babeli. Kwa muhtasari, Kuazari wa Xenophon analingana sana na maelezo ya Dario, Mmedi, katika kitabu cha Danieli. Katika tasnifu yangu, nilifanya uchunguzi wa kina wa vyanzo vingine vya nje vya Biblia ambavyo vinatoa taarifa kuhusu suala la Koreshi na Dario, Mmedi, na nikapata ushahidi thabiti unaounga mkono kuwapo kwa Kuazari II / Dario, Mmedi.


Pingamizi #1: Maandiko ya mikataba ya Babeli ni ya kipindi cha utawala wa Koreshi tangu kuanguka kwa Babeli, bila kuingiliwa na utawala wa Dario, Mmedi.


Majibu: Maandiko ya mkataba pia hayamtaji Belshaza, ambaye Danieli anamtambulisha kuwa sahihi kama “mfalme.” Hii ni kwa sababu maandishi ya mkataba hayataji watawala wote wanotawala pamoja kwa utawala mmoja. Katika suala la uhusiano wa kifalme kati ya Koreshi na Dario, Mmedi, ilikuwa kawaida kunukuu muda wa utawala katika maandishi ya mikataba ya Babeli na utawala wa mfalme aliyeingia Babeli kama mkuu (Koreshi). Walakini, inawezekana kuwa kuna maandishi ya mikataba yaliyowekwa kipindi cha utawala wa Dario, Mmedi, kwani maandishi hayo yangetambuliwa na wasomi wa kisasa na utawala wa mmoja wa Dario watatu ambao walitawala baadaye.


Pingamizi #2: Cyropaedia ya Xenophon sio chanzo cha kuaminika kwa historia ya Koreshi.


Majibu: Tathmini hii ya Cyropaedia inategemea utangulizi kwamba Kuazari II ni uzushi. Ikiwa mtu atakubali uhalisi wa Kuazari II, basi Cyropaedia inaonekana kuaminika zaidi. Kwa kuongezea, Xenophon amethibitishwa kwa usahihi zaidi kuliko Herodoti kuhusiana na maelezo yake juu ya malezi ya kifalme ya Koreshi, kuwapo kwa Belshaza, kuwapo wa Gobryas, na ndoa ya Koreshi na binti wa Kuazari.


Kusoma maelezo zaidi juu ya utambulisho wa Dario, Mmedi, na Kuazari II na vyanzo vya zamani ambavyo vinaunga mkono ufananisho huu, angalia nakala yangu: Darius the Mede: A Solution to His Identity (Dario, Mmedi: Suluhisho la utambulisho wake).

Hakimiliki © 2020 na Steven D. Anderson.


Dk. Steven D. Anderson alipokea udaktari wake (Ph. D.) katika Mafunzo ya Kibiblia na mkusanyiko wa Maonyesho ya Biblia kutoka Seminari ya Theolojia ya Dallas (Dallas, TX).

Español  |  English  |  العربية  |  Français  |  Português  Kiswahili  | русский Norsk  |

bottom of page